Luke 8:40-56

Msichana Afufuliwa, Na Mwanamke Aponywa

(Mathayo 9:18-26; Marko 5:21-43)

40 aBasi Yesu aliporudi, umati mkubwa wa watu ukampokea kwa furaha, kwani walikuwa wakimngojea. 41 bKisha mtu mmoja, jina lake Yairo, aliyekuwa kiongozi wa sinagogi, akaja na kuanguka miguuni mwa Yesu, akimwomba afike nyumbani kwake, 42 ckwa kuwa binti yake wa pekee, mwenye umri wa miaka kumi na miwili, alikuwa anakufa.

Yesu alipokuwa akienda, umati wa watu ukamsonga sana.
43 dKatika umati huo palikuwa na mwanamke mmoja aliyekuwa na tatizo la kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili. Tena alikuwa amegharimia yote aliyokuwa nayo kwa ajili ya matibabu, wala hakuna yeyote aliyeweza kumponya. 44 eHuyo mwanamke akaja kwa nyuma ya Yesu na kugusa upindo wa vazi lake. Mara kutokwa damu kwake kukakoma.

45 fYesu akauliza, “Ni nani aliyenigusa?”

Watu wote walipokana, Petro akasema, “Bwana, huu umati wa watu unakusonga na kukusukuma kila upande.”

46 gLakini Yesu akasema, “Kuna mtu aliyenigusa, kwa maana nimetambua kuwa nguvu zimenitoka.”

47Yule mwanamke alipofahamu ya kuwa hawezi kuendelea kujificha, alikuja akitetemeka, akaanguka miguuni mwa Yesu. Akaeleza mbele ya watu wote kwa nini alimgusa na jinsi alivyoponywa mara. 48 hBasi Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani.”

49 iYesu alipokuwa bado anasema, akaja mtumishi kutoka nyumbani kwa Yairo, yule kiongozi wa sinagogi, kumwambia, “Binti yako amekwisha kufa. Usiendelee kumsumbua Mwalimu.”

50Yesu aliposikia jambo hili, akamwambia Yairo, “Usiogope. Amini tu, naye binti yako atapona.”

51 jWalipofika nyumbani kwa Yairo, hakumruhusu mtu yeyote aingie ndani naye isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana, pamoja na baba na mama wa yule binti. 52 kWakati ule ule watu wote walikuwa wakilia na kuomboleza kwa ajili ya huyo binti. Yesu akawaambia, “Acheni kulia. Huyu binti hajafa, ila amelala.”

53Wao wakamcheka kwa dharau, wakijua kuwa amekwisha kufa. 54 lYesu akamshika yule binti mkono na kuita, “Binti, amka!” 55Roho yake ikamrudia, naye akainuka mara moja. Akaamuru apewe kitu cha kula. 56 mWazazi wake wakastaajabu sana, lakini Yesu akawakataza wasimwambie mtu yeyote juu ya yale yaliyotukia.

Copyright information for SwhNEN